Utafiti mpya uliofanyika nchini Marekani umesema ya kwamba kula machungwa na zabibu kunaweza kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi (Stroke).
Utafiti huo uliangalia faida za matunda chachu (Citrus Fruit) pekee kwa mara ya kwanza tofauti na tafiti nyingi ambazo tumezizoea zinazoangalia umuhimu wa matunda na mboga za majani kwa afya kiujumla.
Utafiti huu umehusisha maelfu ya wanawake wanaoshiriki katika tafiti ya manesi Nurse’s Health Study lakini wataalamu wanaamini faida hizo za machungwa na zabibu pia zinapatikana kwa wanaume.
Timu ya watafiti katika chuo cha Norwich Medical School katika Chuo Kikuu cha East Anglia wamechunguza umuhimu wa kemikali aina ya flavonoidsambayo ni jamii ya antioxidant (kemikali zinauwa kemikali hatari za kwenye mwili) inayopatikana katika matunda, mboga za majani, chocolate nyeusi na wine nyekundu.
Utafiti huu ulifuatilia takwimu za miaka 14 za wanawake 69,222 ambao walikuwa wakishirki katika tafiti kwa kuandika kiwango chao cha kula matunda na mboga za majani kwa kila kipindi cha miaka 4. Timu hiyo ya utafiti iliangalia
uhusiano wa aina sita ya flavonoids - flavanones, anthocyanins, flavan-3-ols, flavonoid polymers, flavonols na flavones na hatari ya aina mbalimbali za kiharusi kama Ischaemic, Hemorrhagic na Total Stroke. Ilionekna wanawake waliokula kiwango kikubwa cha flavanones kwenye matunda chachu walikuwa na asilimia 19 ya uwezekano wa
kupunguza kiharusi kulinganisha na wanawake ambao walikula kiwango kidogo cha matunda hayo.
Kiwango kikubwa cha flavanones kilikuwa 45mg kwa siku kulinganisha na kiwango kidogo cha 25mg kwa siku. Utafiti huu ulichapishwa katika jarida laMedical Journal Stroke umesema flavanones hupatikana kwa asilimia 82 kwenye
machungwa na juisi ya machungwa na hupatikana kwa asilimia 14 kwenye zabibu na juisi ya zabibu. Hata hivyo watafiti hao wamesema kwa wale wenye kusudio la kuongeza kiwango kikubwa cha flavanones itawalazimu kula tunda la chungwa kwa wingi na si juisi za machungwa zinazotengenezwa kiwandani kutokana na kiwango kikubwa cha sukari kinachopatikana katika juisi hizo za viwandani.
Professa Aedin Cassidy wa masuala ya lishe bora (nutrition) na ambaye alikuwa kiongozi wa utafiti huo amesema “kula kwa wingi kwa matunda, mboga za majani, na hasa Vitamin C uhusishwa na kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi”. Flavanones hutoa kinga dhidhi ya kiharusi kutokana na kuongeza ufanisi wa mishipa ya damu kwenye ubongo
na kutokana na kuwa na uwezo wa kuzuia maambukizi mwilini (Anti-inflammatory effect).
Utafiti uliofanyika hapo awali ulionyesha ya kwamba ulaji wa matunda chachu na juisi yake na si matunda ya aina nyingine yoyote hupunguza uwezekano wa kupata kiharusi aina ya Ischaemic Stroke na kuvuja damu kwenye ubongo(Intracerebral Haemorrhage).
Utafiti mwingine uliofanyika kipindi cha nyuma ulionyesha hakuna uhusiano wowote wa matunda ya njano na machungwa katika kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi lakini ulionyesha ya kwamba kuna uhusiano wa zabibu na mapeasi wa kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi.
Katika utafiti mwingine uliofanyika nchini Sweden umeonyesha ya kwamba wanawake ambao walikula kiwango kikubwa cha antioxidant karibia asilimia 50 kutoka kwenye matunda na mboga za majani, ni wachache tu kati yao waliopata kiharusi ikilinganishwa na wanawake ambao walikuwa na kiwango kidogo cha antioxidant.
Matokeo ya utafiti huu yasiwafanye watu kuacha kula matunda ya aina nyingine pamoja na mboga za majani kwani nayo yana faida kubwa katika mwili wa binadamu.
Kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi inawezekana kama mtu atakula lishe bora iliyo na virutubisho vyote muhimu, kula matunda na mboga za majani kwa wingi, kufanya mazoezi mara kwa mara, kupunguza kiwango cha ulaji chumvi (kwani watu wenye asili ya Kiafrika wana kiashiria cha asili kinachojulikana kama salt retention gene ambacho hufanya
kiwango kidogo cha matumizi ya chumvi mwilini kuonekana kama kiwango kikubwa na hivyo kuongeza hatari ya kupata kiharusi), kupunguza uzito (kuwa kwenye uzito unaotakikana kiafya kulingana na umri na urefu wako), kupunguza kiwango cha matumizi ya mafuta katika chakula, kulala masaa ya kutosha na kupunguza msongo wa mawazo.
CREDIT : VYOMBO MBALIMBALI VYA HABARI
Comments
Post a Comment