Watumiaji
wa kilevi cha shisha wako katika hatari kubwa ya kuugua maradhi ikiwemo
saratani na kuathirika katika mfumo wa hewa.
Wataalamu
wa afya wameonya kwamba ulevi huo ambao kwa sasa umeshika kasi na kuteka watu
wengi hasa vijana, una hatari kubwa kuliko uvutaji wa sigara.
Iinasadikiwa
watu wengi, hususani vijana, hivi sasa wameibukia katika uvutaji huo, wakiamini
ndiyo mbadala wa sigara kwa kudhani kuwa haina madhara.
Daktari wa
Kitengo cha Matibabu ya Saratani, Hospitali ya Aga Khan, Dk Amiyn Alidina,
alisema hayo kwenye majadiliano ya ufahamu wa magonjwa ya saratani
yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Dk Alidina
alisema kilevi hicho hakina tofauti na sigara, ambayo mvutaji wake hawezi
kukwepa magonjwa ya saratani, maradhi ya moyo na maradhi ya mfumo wa hewa.
"Shisha
haiwezi kuwa mbadala wa sigara kwa kudhani kuwa mtu hawezi kupata saratani na
magonjwa mengine, hii ni hatari zaidi," alisema.
Ulevi huo
hutengezwa kwa kutumia chombo maalumu chenye bomba la kutolea moshi, ambacho
huwekewa tumbaku, maji na moto huku ikiaminika mvuke husaidia kuchuja nguvu ya
tumbaku inayoathiri mwili.
Kwa mujibu
wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), mkupuo mmoja wa shisha una
kemikali hai 4,800 na kwamba kemikali hizo husababisha saratani ya
mapafu, maradhi ya moyo na matatizo katika mfumo wa hewa.
Taarifa
hizo za WHO zinaeleza kwamba, kiasi cha uvutaji wa shisha kwa saa
moja ni sawa na kuvuta sigara kati ya 100 na 200.
Hii ni
kutokana na kwamba, mvutaji wa sigara hupata mikupuo kati ya minane na 12 ambayo
huingiza lita 0.5 hadi 0.6 za moshi. Lakini kwa upande wa shisha, taarifa hizo
za wataalamu zinaonesha anaweza kuvuta mara 200, kiasi ambacho huingiza kati ya
lita 0.15 hadi moja ya moshi.
Dk Alidina
anafafanua kwamba saratani imekuwa tatizo kubwa ambalo kwa kiasi kingine
huchangiwa na mtindo wa maisha ambao umefanya watu kushindwa kufahamu utaratibu
wa kujikinga.
Wakati huo
huo alisisitiza kwamba iwapo kwenye familia ipo historia ya watu
wenye saratani, inatakiwa kuwa waangalifu zaidi.
Miongoni
mwa mambo ambayo jamii na familia kwa ujumla zinasisitizwa kuzingatia, ni ulaji
wa matunda na kuacha matumizi ya pombe na sigara. Mtaalamu huyo pia
anahimiza kufanya mazoezi ili kujiepusha na hatari ya kuugua saratani.
Wakati
hapa nchini, hususani jijini Dar es Salaam, lipo wimbi kubwa la vijana
wakiwemo wasichana wanaojihusisha na uvutaji wa kilevi hiki katika baa
mbalimbali, vile vile taarifa kutoka maeneo mbalimbali duniani,
zinaonesha kundi hili kutekwa na matumizi ya shisha.
“Uvutaji
wa shisha unazidi kukua kwa sababu watu wengi hawajui madhara yake kama
wanavyofahamu uvutaji wa sigara,” Profesa wa Chuo Kikuu cha London, Robert
West, alikaririwa hivi karibuni na gazeti la Daily Mail la Uingereza.
Comments
Post a Comment