Licha ya jitihada zinazofanywa na wanawake
waishio mjini ikiwamo jijini Dar es Salaam, ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
(NBS) inaonyesha idadi ya wanaoelemewa na uzito inaongezeka.
Ripoti hiyo ya utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya
(NPS) ya mwaka 2020/21 inaonyesha asilimia 47 ya wanawake wenye umri kati ya
miaka 15 hadi 49 wasio na mimba, wana uzito uliopitiliza likiwa ni ongezeko la
asilimia 8.2 kutoka mwaka 2014/15.
Ripoti hiyo iliyotumia kipimo cha ulingano wa
uzito na urefu (BMI) inaonyesha vigezo vya mtu kuwa na uzito uliopitiliza ni
kuwa na BMI kuanzia 25 na zaidi ya 30.
Takwimu hizo zinaonyesha katika kila wanawake
wawili nchini, mmoja ana uzito uliopitiliza kutokana na kutumia vyakula vyenye
mafuta mengi.
Kwa wanawake wanaoishi Dar es Salaam, ripoti
imewaweka katika hali ya hatari zaidi kupata magonjwa ya shinikizo la damu,
kisukari na saratani kutokana na uzito uliopitiliza kwani saba katika kila 10
wana hali hiyo.
“Wanawake wenye uzito uliopitiliza mwaka 2014/15
jijini Dar es Salaam walikuwa asilimia 52.7 lakini wameongezeka hadi asilimia
64.5 mwaka 2020/21,” inasema ripoti hiyo.
Asilimia 40.3 ya wanawake wanaoishi vijijini, ripoti
inasema wana uzito uliopitiliza wakilinganishwa na asilimia 60.5 ya wanawake wa
mjini.
Matokeo ya utafiti huu yanalingana na ule
uliofanyika India mwaka 2013 na kuchapishwa katika Journal of Family Medicine
and Primary Care ulioitwa ‘lishe na shughuli za kimwili miongoni mwa wanawake
katika maeneo ya mjini na vijijini kusini mwa India’ ambao ulionyesha wanawake
wa vijijini hawana uzito uliozidi kutokana na kufanya shughuli za kimwili mara
tatu zaidi ya wanawake wa mjini.
Anastazia Mwelu (27), mkazi wa Sinza jijini Dar es
Salaam mwenye uzito wa kilo 96 anasema ameshauriwa na daktari kuacha kula
vyakula vyenye mafuta na wanga kwa wingi ili kupunguza uzito.
“Nilienda hospitali daktari alinishauri vyakula
ambavyo sitakiwi kutumia kwa sasa zikiwamo chipsi ambazo nahisi
zimenisababishia huu mwili. Pia, nimeambiwa niache kula vyakula vya wanga na
nifanye mazoezi sana,” anasema Anastazia.
Katika hali ya mashaka na kutojiamini, Christina
Joseph, mkazi wa Mbezi Beach jijini humo ana wasiwasi wa kuongezeka uzito
kutokana na kukaa nyumbani muda mwingi baada ya kumaliza masomo yake ya chuo
kikuu.
“Naona kabisa uzito wangu unaongezeka na nakuwa
mvivu kwa sababu sina shughuli za kufanya baada ya kumaliza chuo, nikiamka
asubuhi ni kula, kufanya shughuli za nyumbani na kulala. Naogopa kupima uzito,
nahofu nitakuwa nimeongezeka uzito,” anasema Christina.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika
Hospitali ya Salaaman, Abdul Mkeyenge anasema sababu ya wanawake kuwa na uzito
mkubwa ni kutokula mlo kamili kama inavyoshauriwa.
Kwa kawaida, anasema kila binadamu anatakiwa kuwa
na uwiano kati ya urefu na uzito wa mwili wake yaani BMI.
“Kwa kawaida, BMI inatakiwa kuanzia 18 mpaka 29.5
kwani zaidi ya 30 inamaanisha uzito uliopitiliza. Kuna sababu nyingi za mtu
kuwa na uzito uliopitiliza lakini kubwa ni kutofuatilia mlo kamili,” anasema
daktari huyo.”
Kitu cha msingi kuzingatia anasema ni kuepuka
vyakula vyenye mafuta na sukari kwa wingi ambavyo wanawake wengi wanavipenda
zaidi.
“Mji kama Dar es Salaam unakua kwa kasi na watu
hawapangi ratiba ya kula vizuri, wanapenda kula vyakula vyenye mafuta na sukari
na wanakunywa pombe kupitiliza,” anasema.
Vyakula vinavyoliwa mjini, daktari huyo anasema ni
vya kusindika na huwekwa kwenye friji kwa muda mrefu hivyo kupoteza ubora.
Changamoto iliyopo, Dk Mkeyenge anasema ni mafuta
kwenda kurundikana kwenye mishipa ya damu hali inayochochea uzito na kuzalisha
shinikizo la damu kwa wanawake na wanaume.
Anasema kuzaa hakuna uhusiano wowote na uzito
uliopitiliza kwani mtoto anapotengenezwa tumboni mwili huhitaji chakula kingi
lakini wengi hawali mlo kamili ila wanajaza vyenye sukari na mafuta hivyo
kujikuta wananenepa kupita kiasi baada ya kujifungua.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Isaya
Mhando anasema wanawake wengi huongezeka uzito baada ya kujifungua.
“Kuna sababu nyingi, mama anaweza kuongezeka uzito
pindi kipato kinapoongezeka au kupungua kwa kazi alizonazo lakini wengi wanaingia
kwenye tabia bwete kwa kutokufanya kazi, anatembelea gari akifika nyumbani
anakaa tu kwenye kochi,” anasema.
Wanawake wengi, Dk Mhando anasema hawali vyakula
vya asili na hawana elimu ya lishe bora.
“Kuna utafiti ulifanyika Kilimanjaro ulioonyesha kuna
ongezeko la wanawake wenye vitambi huku kipato nacho kikiongezeka na maeneo
yanayozalisha chakula ilionekana kuna watoto wana utapiamlo,” anasema Dk Mhando.
Utapiamlo, anasema huweza kujidhihirisha kwa kuwa
na uzito kidogo au uliopindukia hivyo ni lazima watu wakafahamu wanapaswa kula
vyakula gani na kufanya mazoezi na au kazi zinazoushughulisha mwili ikiwamo
kulima.
Lishe bora
Ofisa Lishe Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya
Chakula na Lishe (TFNC), Walbart Mgeni anasema ni muhimu kila mtu kula mlo kamili
ili kusaidia umeng’enywaji na ufyonzwaji wa chakula.
Kila mlo kamili, anasema unatakiwa kuwa na makundi
yote matano ya vyakula vikiwamo vya nafaka, mizizi na matunda, mbogamboga,
jamii za kunde na vyenye asili ya wanyama, mafuta na sukari bila kusahau kunywa
maji safi.
“Tunachosisitiza mlo utokane na makundi hayo kwani
unapokula zaidi sukari na mafuta unasababisha mwili kuongezeka. Wanawake wengi
wanapenda vyakula hivyo kuliko wanaume,” anasema.
Mtaalamu wa Lishe wa Hospitali ya Taaluma na Tiba
Mloganzila, Theresia Thomas anasema mlo kamili unatakiwa kuwa na mchanganyiko
wa mbogamboga na matunda ambavyo huongeza kinga za mwili.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Saratani wa Hospitali ya
Aga Khan, Dk Harrison Chuwa anasema ulaji usiofaa husababisha saratani ya mfumo
wa chakula.
Dk Chuwa anasema miaka ya hivi karibuni wanapokea
wagonjwa wengi wa saratani ikilinganishwa na miaka ya nyuma kutokana na mfumo
mbaya wa maisha.
“Saratani hizi nyingi zimetokana na kula vyakula
vya mafuta, kunywa pombe kali na kutofanya mazoezi,” anasema Dk Chuwa.
Credit : NBS TANZANIA/ MWANANCHI
Tatizo la
kitambi linaweza kuthibitiwa kwa
kutumia dawa mbalimbali za
asili. Kufahamu namna tatizo la
kitambi linavyo weza kudhibitiwa
kwa kutumia dawa za
mimea ya asili, bonyeza link hii
hapa chini :
https://neemaherbalist.blogspot.com/2015/11/fahamu-jinsi-kitambi-kinavyo-patikana.html
Comments
Post a Comment