Grace Simon mwenye miaka 14 anateseka na uzito.
GRACE Simon mwenye miaka 14 anateseka na uzito wa kupindukia wa
kilo 111 (kama gunia moja la mahindi na viroba vitatu) hali iliyomsababishia
akatishwe masomo na walimu katika Shule ya Msingi Amani, Ukonga, Ilala jijini
Dar es Salaam alikokuwa anasoma.Grace ambaye mwaka huu angekuwa darasa la saba
lakini aliachishwa shule mwaka 2010 akiwa darasa la nne na walimu wakimtaka akatibiwe.
MAMA MZAZI ASIMULIA
Akizungumza na Uwazi kuhusu mkasa mzima wa mtoto Grace, mama yake mzazi,
Ashura Bakari alisema binti yake alimzaa salama mwaka 2000 lakini ilipofikia
mwaka 2002 akiwa na miaka miwili alianza kuvimba tumbo hali ambayo hakujua
chanzo chake.
ATENGWA NA WANAFUNZI
Mama huyo akizungumza kwa masikitiko alisema kuwa, Grace alipofika darasa
la nne, akiwa na umri wa miaka kumi baadhi ya wanafunzi wenzake walianza
kumnyanyapaa kutokana na unene ambao ulikuwa ukiongezeka siku hadi siku.
“Walikuwa wakimtania sana mwanangu hadi kukosa amani. Hali hiyo
iliwafanya walimu kumsimamisha masomo ili atibiwe. Hadi sasa sijapata msaada wa
kupona kwake,” alisema mama huyo huku machozi yakimtoka.
HOSPITALI ZIMESHINDWA?
Aidha, mama Grace aliongeza kuwa amekwishahangaika katika hospitali
mbalimbali za jijini Dar es Salaam, ikiwemo Muhimbili bila mafanikio.
“Muhimbili waliniambia ili mwanangu aweze kufanyiwa vipimo pamoja na
matibabu gharama zake ni shilingi laki nane (800,000) ambazo nimezikosa na hakuna
mtu wa kunisaidia,” alisema.
NDUGU NAO
Alisema mbali na kutafuta tiba hospitalini, amekuwa akipita huku na huko
kuomba msaada wa fedha kutoka kwa ndugu na jamaa lakini hakuna aliyemsadia.
KWA NINI BABA MZAZI ASIMSAIDIE?
Katika hali ya kushangaza, mama huyo alisema ili kupata fedha hizo
anahangaika peke yake kwa sababu baba mzazi wa Grace, Simon alikataa kutoa
msaada wowote.
“Baba yake yupo hai, alikuwa anatoa msaada kipindi cha mwanzo lakini
miaka kama mitano imepita hakuna msaada anaonipa. Ni kweli hatuishi pamoja
lakini mtoto tulizaa wote,” alisema kwa masikitiko makubwa mama huyo.
WALICHOKIONA MADAKTARI
Akizungumzia kiini cha tatizo, mama huyo alisema: “Kwa mujibu wa
madaktari mwanangu anasumbuliwa na moyo kujaa mafuta mengi, kwa hiyo homoni
zake zimekosa uwiano na ini pia lina sumu nyingi.”
GRACE AWALILIA WATANZANIA
Akizungumza na mwandishi wetu, mtoto huyo anayetamani kuendelea kusoma
aliwaomba Watanzania wamsaidie fedha ili aweze kutibiwa na kurejea darasani.
“Niliachishwa shule ili nitibiwe, nikipona nirejee shuleni, lakini hadi
sasa sijapata nafuu, na ninajua ni kutokana na kutopata matibabu sahihi,”
alisema Grace huku akilia.
UONGOZI WA SHULE
Mmoja wa walimu waandamizi wa Shule ya Msingi Amani alipokuwa akisoma mwanafunzi
huyo (hakuwa tayari kutaja jina lake), alikiri kumtambua mwanafunzi huyo
na kusema aliachishwa shule kwa hofu ya uongozi wa shule.
“Hatukumwachisha shule kwa nia mbaya, lakini lengo letu lilikuwa
akatibiwe kisha arudi shuleni lakini matibabu anayopata hajaweza kupona na hali
aliyokuwa nayo inazidi kuongezeka siku hadi siku,” alisema mwalimu huyo.
Akaongeza: “Mwaka huu Grace ilikuwa awe darasa la saba, lakini hata
kutembea ni tatizo hali ambayo tuliona kuwa unene ule si afya bali ni ugonjwa.”
MSAADA UNAAOHITAJIKA
Kwa yeyote aliyeguswa na tatizo la Grace ambaye anasaka shilingi laki
nane tu ili atibiwe, anaweza kuwasiliana na mama yake mzazi kwa simu:
0719 465445, ASHURA BAKARI.
CREDIT : GLOBALPUBLISHERS
Comments
Post a Comment