Nicklas Bendtner
MSHAMBULIAJI WA Arsenal Nicklas Bendtner Jumatano usiku wiki iliyopita alifunga bao maridadi la kwanza la kuongoza la Arsenal katika pambano dhidi ya Hull City na kuendelea kuiweka kileleni timu yake hiyo ambayo imekuwa ikimsugulisha benchi.
Bendtner alivaa jezi ya Arsenal na kuanza mechi kwa mara ya kwanza ikiwa zimepita siku 1,005 tangu alipoanza mechi yake ya mwisho Emirates kabla ya kutimka kwa mkopo katika klabu za Sunderland na Juventus.
Alibakizwa na kocha wa Arsenal , Arsene Wenger katika siku ya mwisho ya uhamisho wa wachezaji England baada ya kocha uyo Mfaransa kumkosa mshambuliaji wa Chelsea, Demba Ba al;iyekuwa anatarajia kutimka kwa mkopo klabuni hapo.
Hilo lilikuwa bao lake la kwanza tangu alipo fanya hivyo Machi 2011 huku akikosa mabao ya wazi katika pambano la kombe la Ligi dhidi ya West Brom.
Hata hivyo, bao hilo limezua kasheshe kubwa katika mitandao ya kijamii baada ya watu wengi kuanza kumkejeli kutokana na kukaa miaka mingi bila ya kufunga.
Mtu wa kwanza kumkejeli Bendtner alikuwa mshambuliaji wa zamani wa Tottenham na timu ya taifa ya England, Gary Lineker. Huyu aliandika katika akaunti yake ya Twitter akisema “ Baadhi ya washambuliaji mahiri Ligi Kuu England wanafunga mabao leo. Suarez, Aguero na Bendtner “
Alifanya hivi wakati akijua wazi kwamba kwa sasa, Bendtner hachukuliwi kama mshambuliaji hatari katika Ligu Kuu England, achilia mbali ukweli kwamba hafikii kabisa katika anga za Luis Suarez na Sergio Aguero.
Shabiki mwingine wa soka aliyejulikana kama Nooruddean akitumia akaunti yenye jina la @ BeardedGenius alitumia ujumbe akisema “ Chamakh amefunga jana, Bendtner amefunga leo, kesho ni mwisho wa dunia “
Alikuwa akimaanisha bao lililofungwa na mshambuliaji wa Crystal Palace, Maroune Chamakh, Jumanne usiku katika pambano dhidi ya West Ham, huku pia akilikejeli bao la Bendtner dhidi ya Hull City.
Mtandao wa kituo cha BBC cha Uingereza nao uliandika ukweli ambao ulionekana kama kejeli. Wao waliandika “ Nicklas Bendtner amefunga mabao mengi mwezi huu kuliko Christiano Ronaldo, Lionel Messsi, Franck Ribbery na Robin Van Persie ukiwajumlisha pamoja ‘
Ni kweli kwamba mastaa wote hao hawajafunga bao lolote tangu mwezi huu wa Desemba uanze kutokana na kuwa majeruhi, lakini ujumbe huu ulitumwa kama kejeli kwa Bendtner.
Shabiki aliyefahamika kwa jina la Rich B naye alituma ujumbe ulio kuwa na lengo la kumkejeli Bendtner. Yeye aliandika akidai “ Bendtner amefunga bao dhidi ya Hull. Suarez hakuweza kuwafunga. Kwa hiyo Bendtner ni bora kuliko Suarez ‘
Shabiki mwingine aliye itwa Christa naye alitoa kali ya mwaka baada ya kutuma ujumbe katika mtandao wake wa Twitter akionesha kumkejeli mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Denmark.
Christa alisikika akisema :
“ Nimeamka leo asubuhi katika dunia ambayo Nicklas Bendtner amefunga bao. Na ndio maana upepo unavuma kwa kasi sana, nadhani ulimwengu umetingishika vibaya sana”
Wakati Christa akiwa ametoa kejeli hiyo, shabiki mwingine wa Arsenal aliyetambulika kwa jina la Faisal alituma ujumbe wa kejeli ambayo uliashiria kuwa Bendtner alikuwa anastahili kuwa mwanasoka bora wa dunia.
“ Jina Bendtner huwa linaanza na herufi B na huwa linaishia na herufi R, hii ni kama ilivyo jina la BALLON D’OR, aliandika Faisal kwa kejeli kubwa.
Shabiki mmoja aliyejulikana kwa jina la Ken alikwenda mbali zaidi baada ya kumlinganisha Bendtner na mastaa wa zamani wa Arsenal, Dennis Bergkamp na Thiery HENRY.
“ Bergkamp kisha Henry…na sasa Bendtner !”
Ameonyesha jinsi alivyo bora katika kufunga pindi anaporudi uwanjani kwa namna ya kushindana na wakongwe hawa “
Faraja pekee ambayo Bendtner ameipata ni kutoka katika kauli ya nahodha wake, Mikel Arteta ambaye alisema staa huyo mwenye majigambo bado ni mchezaji muhimu katika kusaka ubingwa wa England.
“ Hicho ndicho tunacho taka. Wachezaji waliopo kikosini wanaweza kuchangia timu kupata mafanikio. Kila mtu ni muhimu. Tunamuhitaji kila mmoja kama tunataka kushinda kitu. Nadhani ni kitu kizuri. “ Bado ni mchezaji wa Arsenal na wakati akiwa hapa atatoa asilimia 100 ya nguvu zake. Hatafikiria tofauti au kufanya tofauti” alisema Arteta.
CHANZO : GAZETI LA MWANASPOTI, TOLEO Na. 1440, Desemba 9, 2013.
|
Comments
Post a Comment