Mchungaji Harris Kapiga. |
SIKU ya kupeana zawadi , maarufu kama Boxing Day, ambayo huangukia Desemba 26, kila mwaka, zamu hii itakuwa ya kipekee kwani itaambatana na uzinduzi wa Klabu ya Usiku (Night Club )
Iliyo anzisha na Mchungaji mmoja katika maeneo ya Mbezi Beach, jijini Dar Es salaam, imefahamika.
Kwa mujibu wa Mchungaji huyo, Harris Newman Kapiga, ingawa klabu hiyo itakuwa baadhi ya vifaa kama vilivyo katika klabu za usiku za kidunia, ikiwa ni pamoja na taa za rangi zinazo badilika badilika, kutakuwa na ibada moto moto za kusifu na kuabudu.
“ Sio mikesha, ni Night Club ( Klabu ya Usiku ), na kutakuwa na kiingilio kidogo. Tunataka kutumia muda ambao shetani anautumiwa kuabudiwa, na sisi tumwabudu Mungu wetu “ alisema Mchungaji Kapiga, alipo ongea na Nyakati kwa njia ya simu wiki iliyopita.
Kapiga ambaye pia ni mtangazaji wa Redio ya Clouds ya jijini Dar Es salaam, na pia ni mchungaji wa kanisa maarufu la Nchi Ya Ahadi, alisema klabu hiyo inayoitwa Ela Gospel Club, itazinduliwa rasmi Desemba 26, 2013, siku ya pili baada ya Krismasi.
Alieleza kuwa, jina hilo la “ Ela” linatokana na jina jina la bonde ambalo Daudi alimwangamiza Goliathi, na kwamba anaamini huduma hiyo ya usiku itaangusha Goliathi wengi.
Mchungaji Kapiga, alisema klabu hiyo itakuwa n inafunguliwa kuanzia saa tatu za usiku na kufungwa saa kumi za usiku, na itafanya kazi siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.
“ Watu wasio elewa sasa, wanaweza kuniita Freemason, lakini si lazima wote waelewe wakati mmoja, wataelewa taratibu. Unapoanzisha kitu kipya, usitegemee watu wote wakupigie makofi “, alisema Kapiga alipoulizwa iwapo hiyo isingemfanya aonekane mtu wa ajabu.
Mchungaji Kapiga, alisema klabu ya aina hiyo siyo ya kwanza duniani ingawa itakuwa ya kwanza kwa hapa nchini.
Alisema zipo klabu za aina hiyo Ulaya na hata Marekani pia.
Alisema katika ukumbi wa klabu hiyo ulioko karibu na Shule ya Msingi Mwalimu Nyerere, eneo la Tangi Bovu, kutakuwa na kucheza nyimbo za injili, kutakuwa na nyama choma na mambo kama hayo, isipokuwa pombe, na kwamba mara kadhaa itatolewa nafasi kwa ajili ya wanao taka kuokoka, na wanao hitaji maombezi.
“ Tumewalenga zaidi vijana kati ya miaka 19 hadi 25, ingawa hatuwazuii wenye umri zaidi ya hapo ‘, alisema Kapiga na kuongeza “ Tunataka hawa wa umri wa kujirusha, ila wazee na hata watu wa dini nyingine waje tu, ila wajue habari za Yesu zitakuwapo.
CHANZO : GAZETI LA NYAKATI, TOLEO Na.680, Desemba 08-14, 2013
Comments
Post a Comment