Panadol |
Watu wengi wana mtizamo kuwa dawa zinazouzwa katika
maduka ya dawa baridi na maduka ya kawaida ya vyakula, yaani zile ambazo
hazihitaji agizo la daktari ( over-the-counter (OTC) drugs ) ni salama.
Ukweli
ni kwamba hali haiko hivyo kabisa. Nyingi ya dawa zilizoko katika kundi hili
huko nyuma zilikuwa ni miongoni mwa zile zilizosimamiwa na kuratibiwa kwa
karibu, huku zikitolewa tu kwa agizo la daktari.
Pamoja na kuondolewa katika kundi la dawa zinazohitaji
kutolewa kwa agizo la daktari, bado dawa za OTC ni kemikali ambazo mara nyingi
haziondoi kiini cha tatizo ulilonalo, na zinaweza kukupelekea kupata madhara
makubwa, ikiwa ni pamoja na kifo.
Mfano
mmoja wapo ni dawa ya panadol, ambayo pia hujulikana kama paracetamol,
acetaminophen, tyenol, nakdhalika.
Panadol
ni dawa maarufu kweli kweli. Ni dawa maarufu hasa kutokana na uwezo wake wa
kutuliza maumivu na pia kushusha homa haraka.
Watu wengi hunywa panadol bila ya kujiuliza chochote
kuhusu usalama wake. Kupitia kwa wazazi na walezi wao, watoto wengi sana pia ni
wabugiaji wa dawa hii.
Hii ni
kutokana na wazazi/walezi wao kuamini kuwa kila mtoto anapolia basi mtoto ana
maumivu, na au kila anapopata homa basi kuna ulazima wa kuishusha homa hiyo.
Kwa kiasi kikubwa tabia hii imejengwa na madaktari na
wafamasia ambao nao hutoa dawa hii kwa wagonjwa bila kuzingatia usalama wake,
na hivyo bila kutoa ushauri wowote kana kwamba dawa hizi ni salama kama maziwa!
Hatuna miundo mbinu ya kubaini idadi ya watu
wanaoudhuriwa na matumizi haya ya kiholela ya panadol, lakini kwa kuangalia
takwimu za nchi nyingine, bila shaka watu hao watakuwa ni wengi sana.
Nchini
Marekani utumiaji uliopindukia wa panadol (overdose) umetambuliwa kuwa ndio
sababu kuu ya simu zinazopigwa kuomba msaada katika vituo vya udhibiti wa sumu
(Poison Control Centers) nchini humo, kila mwaka.
Panadol
pia inatuhumiwa kuwa kila mwaka inasababisha kiasi cha watu zaidi ya 56,000
kupatiwa matibabu ya dharura, watu 2,600 kulazwa hospitalini, na kiasi cha watu
458 kupoteza maisha, katika taifa hilo. Sababu ya madhara haya inatajwa kuwa ni
kushindwa kwa kiwango cha juu kwa ini kufanya kazi.
Taasisi ya chakula na dawa ya Marekani (US Food and Drug
Administration (FDA)) mnamo mwaka 2009 ilitoa maelekezo kuwa vifungashio vya
dawa hii viwekewe onyo kuhusu uwezekano wa dawa hii kuharibu ini la mtumiaji.
Hatua
hii ilikuja miaka 32 baada ya jopo la wataalamu kutoa ushauri kwa FDA kuwa onyo
hili lilikuwa ni suala la ‘lazima’!
Katika hatua nyingine, kwa nia ya kupunguza madhara,
mnamo tarehe 14 Januari, 2014 FDA ilitoa kauli iliyokuwa ikiwahimiza wataalamu
wa afya kuacha kuandika maagizo ya dawa (prescriptions) kwa dawa mchanganyiko
ambazo miongoni mwake kulikuwa na vidonge (au vimiminika) vilivyokuwa na
kiambata cha panadol kilichokuwa kikifikia kiasi cha miligramu 325.
Ni vizuri kuzingatia kuwa baadhi ya dawa za maumivu zinazotolewa kwa maagizo ya daktari kama vile Vicodin na Percocet, pia zina kiambata cha panadol na kwa hivyo hazipaswi kuchanganywa na dawa zingine zenye kiambata hiki.
Ni vizuri kuzingatia kuwa baadhi ya dawa za maumivu zinazotolewa kwa maagizo ya daktari kama vile Vicodin na Percocet, pia zina kiambata cha panadol na kwa hivyo hazipaswi kuchanganywa na dawa zingine zenye kiambata hiki.
UTUMIAJI WA PANADOL WAKATI WA UJA UZITO UNAWEZA KUCHOCHEA
UGONJWA WA UTUKUTU MKUBWA KWA WATOTO (Attention Deficit Hyperactivity Disorder
–ADHD)
Hivi sasa kuna kundi la watafiti ambao wanahoji matumizi
ya panadol kwa kina mama wajawazito.
Hoja yao
ni kwamba matumizi ya dawa hii katika kipindi cha ujauzito yanaweza kusababisha
mtoto atakayezaliwa kuwa na tabia ya utukutu uliokithiri.
Matokeo ya utafiti yaliyochapishwa katika jarida la JAMA
Pediatrics, yanaonyesha kuwa panadol ni kitibua homoni ( hormone disruptor), na
uwepo wa homoni usio wa kawaida mwilini wakati wa ujauzito unaweza kuathiri
maendeleo ya kukua kwa ubongo wa mtoto anayeendelea kubadilika na kukua
tumboni.
Utafiti huu ambao ulijumuisha takwimu zilizohusisha zaidi
ya kina mama na watoto 64,000 kutoka katika kituo cha Taifa cha Kujifungulia
cha Denmark (Danish National Birth Cohort), ulionyesha kuwa zaidi ya 50% ya
wanawake waliohusishwa walitoa taarifa za kutumia panadol wakati wakiwa waja
wazito.
Utumiaji
huu wa panadol kwa wanawake hao olionyesha matokeo yafuatayo:
• Ongezeko la 30% la hatari ya mtoto kukumbwa na ADHD katika miaka saba ya kwanza ya maisha yake.
• Ongezeko la 37% la hatari ya mtoto kukumbwa na ugonjwa wa hyperkinetic disorder (HKD), ambao ni aina ya ADHD iliyopindukia mipaka.
Utafiti pia ulibaini kuwa kiwango cha madhara
kilitegemeana na dozi. Kadri mama mjamzito alivyotumia panadol kwa wingi wakati
wa ujauzito ndivyo jinsi ambavyo uwezekano wa mtoto kukumbwa na magonjwa yenye
uhusiano na ADHD ulivyoongezeka.
Aidha kwa mujibu wa utafiti huu watoto wa wanawake ambao walitumia panadol kwa majuma 20 au zaidi wakati wa ujauzito walikuwa na kiwango karibu mara mbili cha hatari ya kukutwa na ugonjwa wa HKD.
MADHARA MENGINE YA KIAFYA YANAYOHUSISHWA NA MATUMIZI YA
PANADOL
Ukiondoa uharibifu wa ini, panadol pia imehusishwa na
madhara mengine ya hatari kama uharibifu wa figo pale inaponywewa na pombe,
saratani za damu, madhara yanayopelekea ngozi kukumbwa na magonjwa kadhaa kama
Stevens-Johnson Syndrome (SJS), toxic epidermal necrolysis (TENS), na acute
generalized exanthematous pustulosis (AGEP), na kuzuia chanjo zisifanye kazi
vizuri pale vinapotumiwa pamoja..
KUDHIBITI MAUMIVU
Kwa kuwa watumiaji wengi wa panadol, hasa kwa watu
wazima, hufanya hivyo kwa nia ya kupambana na maumivu, ni muhimu wakajifunza
mbinu salama na mbadala za kuondoa hayo maumivu.
Moja ya
mbinu mujarabu sana katika suala hili ni kuhakikisha kuwa muda wote mwili wako
haukabiliwi na uhaba wa maji. Mwili wako unapokabiliwa na uhaba wa maji akili
iliyoko mwilini mwako inawasha mfumo wa mgawo wa maji kidogo yaliyoko ndani ya
mwili, ili kuzuia shughuli muhimu zinazotakiwa kuendelea mwilini zisije
zikasimama.
Mfumo
huu huratibiwa na kusimamiwa na homoni ya HISTAMINE, ambayo kunapokuwa na haja
ya mgawo mwili huizalisha kwa wingi.
Kwa
bahati mbaya ni kwamba katika harakati za kufanya kazi yake homoni hii pia
huzalisha kiasi fulani cha maumivu katika maeneo mbalimbali ya mwili.
Ukiondoa uhaba wa maji mwilini, pia viko aina ya vyakula
ambavyo huuchochea mwili kuzalisha kiasi kikubwa cha HISTAMINE.
Ulaji wa
vyakula hivi ni kichocheo kikubwa cha maumivu ndani ya mwili kwa muda wote.
Mungu
akipenda katika post yetu ijayo tutaviongelea vyakula hivi kwa kina.
Tatizo lingine linalosababisha maumivu mwilini ni seli za
mwili kukumbwa na mfuro/uvimbe mwako (inflammation) kutokana na baadhi ya
vyakula tunavyokula, au kutokana na kuugua ugonjwa wowote ule.
Mfuro/uvimbemwako
ni zao la kinga za mwili pale zinapoingia katika mapambano na magonjwa
mbalimbali.
Mfuro/uvimbemwako unapotokea kwa muda mfupi tu siyo
tatizo sana.
Tatizo
linakuwa pale ambapo mfuro/uvimbemwako huo umekuwa ni kitu cha kudumu.
Miongoni
mwa dawa nyingi za kifamasia utakazopewa na daktari wako kwa ajili ya maumivu
ni zile zinazolenga kuzuia mfuro/uvimbemwako.
Hata
hivyo kutokana na dawa nyingi za kifamasia kuwa na usalama unaotia shaka ni
bora mtu ukajaribu njia za asili (natural) za kuzuia mfuro/uvimbemwako.
Upunguzaji wa vyakula vya wanga, hususan vile
vilivyochakatuliwa, na upunguzaji wa matumizi ya mafuta ya kupikia yanayotokana
na mbegu (polyunsaturated fats) ni moja ya njia nzuri sana za kudhibiti hali
hiyo.
Baadhi
ya vitu vinavoliwa pia ni visawazishaji vikubwa vya mfuro/uvimbemwako.
Hivi ni
pamoja na chai ya kijani (green tea), manjano (turmeric), karafuu, vitunguu
saumu, matunda ya jamii ya berries (mfano zambarau), zabibu, na vitamini C.
Tatizo lingine linalosababisha maumivu ni makovu
yanayojitokeza ndani kwa ndani mwilini kufuatia kuumia kwa tishu mbalimbali
ndani ya mwili.
Ulaji wa
vyakula vyenye vimeng’enya vyenye uwezo wa kuyeyusha makovu hayo (proteolytic
enzymes) ni njia moja mujarabu sana katika kupambana na maumivu ya aina hii.
Bromelain ni kimeng’enya kinachopatikana katika kigogo
cha katikati ya tunda la nanasi. Kimeng’enya hiki kimebainika kuwa na nguvu
sana katika kufanya kazi hii.
Kimeng’anya
kingine kinachpatikana katika matunda ambacho pia kinaweza kufanya kazi kama
bromelain ni papain.
Papain
ni kimeng’enya kinachopatikana kwa wingi katika tunda la papai.
Sababu nyingine kubwa ya maumivu ndani ya mwili ni
kemikali zinazoitwa prostaglandins.
Prostaglandins
ni kemikali muhimu sana katika kuratibu shughuli kadhaa za baadhi ya viungo
ndani ya mwili kama vile utambuzi wa maumivu, upanukaji na usinyaaji wa mishipa
ya damu, ufanyaji kazi wa mafigo, ufanyaji kazi wa mfumo wa uzazi wa mwanamke,
ufanyaji kazi wa utando wa ndani wa njia ya chakula, nakadhalika.
Kutokana na moja ya kazi za prostaglands kuwa ni utambuzi
wa maumivu, basi mfumo wa tiba za kisasa huchukulia kwamba kemikali hizi ni
moja ya vyanzo vikubwa vya maumivu, na zimebuniwa dawa nyingi za kuzuia mwili
kuzalisha kemikali hizi, au kuzizuia zisifanye kazi pale ambapo tayari ziko
mwilini! Moja ya dawa maarufu sana katika suala hili ni asprin.
Tafiti za kisasa zinaonyesha kuwa asprin inafanya kazi
hii kwa weledi mkubwa mno kiasi kwamba inafikia kuharibu seli za utando wa
ndani wa njia ya chakula na kumsababishia mtumiaji vidonda hatari vya tumbo!
Hata hivyo tafiti pia zimebaini kuwa kiungo cha tangawizi ni mujarabu sana na
salama katika kudhibiti maumivu yanayooanishwa na prostaglandins. Chai ya
tangawizi ya moto itakuondolea tatizo hili na kukuacha huru bila maumivu,
lakini pia ukiwa salama kabisa.
Mbinu ingine ya asili na salama inayotumika kutuliza
maumivu, hasa ya misuli, ni kutumia losheni au cream zenye kiambata cha
menthol. Menthol ni kemikali inayochujwa kutoka katika kiziduo cha mmea
unaoitwa mint au pepper mint. Losheni au cream yenye menthol hupakwa kwenye
eneo lenye maumivu.
Menthol inapenya na kuingia ndani ambapo hupelekea
mishipa ya damu katika eneo hilo kupanuka na kuongeza mtiririko wa damu katika
eneo hilo. Kutokana na hali hii kemikali na virutubisho vinavyohitajika kufika
katika eneo hilo na kurekebisha tatizo hufika kwa wingi ndani ya muda mfupi na
kufanya kazi yake. Menthol pia hujenga mazingira ya kufanya eneo husika lijione
kama limeingiwa na ubaridi. Ubaridi huu hupelekea kupoozwa kwa hali ya
kujisikia moto kunakozalishwa na mfuro/uvimbe mwako katika eneo hilo.
KUDHIBITI HOMA
Tofauti na inavyodhaniwa na watu wengi, homa ya kawaida
siyo kitu kibaya. Homa inakuwa tishio tu pale joto la mwili linapopanda sana na
kuzidi nyuzi joto 104 katika kipimo cha Fahrenheit sawa na nyuzi joto 40 katika
kipimo cha Celcius.
Homa ni silaha inayotumia pia na kinga za mwili katika
jitihada za kukulinda. Vimelea vingi vya maradhi havina uwezo wa kuishi mwilini
na kuzaliana katika joto la mwili linalofikia nyuzi joto hizi. Joto la mwili
linapozidi nyuzi joto hizi kunakuwa na hatari ya kuzuka kwa uharibifu wa
protini za mwili, haswa vimeng’nya pamoja na mafuta ya mwili.
Kutokana na hali hii ni vizuri kuisimamia homa yoyote kwa
ukaribu kuhakikisha kuwa joto haliendi nje ya mipaka iliyokusudiwa. Homa yoyote
ambayo joto litakuwa ndani ya mipaka iliyokusudiwa itakuwa ni msaada mkubwa kwa
mgonjwa katika kuhakikisha kuwa anapona haraka.
Ni vizuri kuwa na kipima joto nyumbani kwa ajili ya kazi
hiyo, badala ya kukimbilia kunywa panadol kila tunapoona kuwa homa imepanda.
Kupitia kipima joto tukiona kuwa homa inataka kupindukia mipaka ni vizuri
kutumia sponji au kitambaa kilicholowekwa kwenye maji ya baridi kumkanda
mgonjwa na pia kumpa maji ya kunywa ya kutosha. Mbinu hii itasaidia kushusha
joto la mwili la mgonjwa bila kumsababishia madhara. Dawa kama panadol zitumike
tu pale ambapo jitihada nyingine zote za kurejesha joto katika hali ya kawaida
zimeshindikana.
Credit : HERBAL IMPACT
Comments
Post a Comment