Watu wengi wanao pata ajali za barabarani na kuvunjika viungo vya mwili ni nadra sana kukimbilia kwa wataalamu wa tiba a silia.
Goodluck Eliona na Warioba Igombe, Gazeti la Mwananchi.
Morogoro na Dar Es salaam.
Watanzania walio wengi hukifahamu kitengo cha mifupa cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ( MOI ) kuwa ni kimbilio muhimu kwa watu walio vunjika mifupa ya viungo vyao.
Lakini kuna idadi kubwa ya waganga wa tiba asilia wanao dai wana uwezo wa kuunganisha mfupa ulio vunjika na wanaaminika sana.
Hata hivyo tiba hiyo ya asili inakinzana na utaalamu wa tiba za kisasa.
Idadi ya watu wanao amii uponyaji wa mifupa unao fanywa na waganga wa jadi inaonekana kuzidi kuongezeka .
Lakini tiba hiyo hufanywa bila ya kufahamu ukubwa wa tatizo. Ni wapi wanapo kinzana ?
AONAVYO MGANGA WA TIBA ASILIA
Joel Kisome ( 57 ), mtaalamu bingwa wa mifupa anaye ishi Morogoro, anaeleza kuwa anatibu mifupa iliyo vunjika akitumia mitishamba.
Uwani mwake kuna zaidi ya wagonjwa 150 ambao wamevunjika mifupa sehemu mbalimbali za miili yao.
“ Sisi hatuna elimu ya kisayansi kama walivyo wenzetu wazungu, lakini Mwenyezi Mungu alitujaalia taaluma hii inayo wasaidia watanzania wenzetu” anasema.
Laiti nasi tungekuwa tumeelimika kisayansi, naamini tungefika mbali hasa katika tiba ya mitishamba.
“ Mzungu humpima mwanaye na kujua kitu anachopenda kukifanya kimaisha tangu akiwa mdogo na kumwendeleza kielimu ili kukuza kipaji chake kitaaluma kwa kile anachokipenda tofauti na waafrika “
Hata hivyo Kisome anaeleza kuwa tiba ya asili inaweza kuwasaidia watu wengi ndani na nje ya nchi, tatizo ni kwa wataalamu wake kutothaminiwa na kusaidiwa na serikali.
Kisome anasema aliianza kazi hiyo ya tiba mwaka 1972 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani baada ya kuonyeshwa dawa hizi na baba yake mzazi, ambaye pia alikuwa mganga mahiri wa tiba asili wa matatizo ya mifupa. Anasema ukaribu na baba yake mzazi ndio ulio mwezesha kurithi kazi ile.
NI WAPI HUPATA WATEJA ?
Kisome hupata wateja wengi kutoka hospitalini, zikiwamo za Muhimbili au Bugando. Wagonjwa wengi wao wakiwa wale wasio na uwezo wa kugharimia tiba zao.
Hata hivyo anaeleza kuwa wagonjwa ni wengi kiasi kwamba wengine hawezi kuwahudumia.
Kuhusu yeye kufanya kazi hospitalini kusaidiana na wataalamu wa tiba ya ya kisasa kuokoa maisha ya wagonjwa, Kisome anajibu kuwa hawezi kufanya hivyo ingawa wamekuwa wakimhitaji.
Anasema hapendi wala hawezi kufanya hivyo kwa kuwa hatakuwa huru.
Anaeleza kuwa serikali haiwezi kumpa fedha anazo hitaji mbali na kufanya katika mazingira magumu, lakini pia hatakuwa na muda wa kupumzika.
ASEMAVYO MTEJA WAKE
Hosel Juma ambaye amepachikwa jina la utani “ Moi” kwa kuwa alikaa Muhimbili kwa mwaka mmoja na miezi minane bila nafuu, anasema kuwa tiba za asili ni bora kuliko zile za hospitalini.
“ Nimekaa Muhimbili ( Moi ) kwa mwaka mmoja na miezi minane bila kupata hata nafuu. Nimetumia fedha zangu zaidi ya Sh. 2 milioni, lakini ni kama nilizitupa “ anasema Juma.
Anaeleza kuwa alipata ajali ya gari alipokuwa amepewa lifti na kuvunjika mguu na alipofikishwa Moi alipigwa picha ya x-ray mara 62, kufungwa bandeji ngumu ( P.O.P ) mara kumi, kuwekewa vyuma mara mbili bila nafuu.
“ Mungu mkubwa! Mbali na kupigwa x-ray, kuwekewa antenna ( chuma mguuni ) na POP kwa muda mrefu wakati nikiwa Muhimbili, sikupata nafuu.
Tangu nilipoletwa hapa kwa mganga na mama mdogo anaye ishi Morogoro, nina miezi mitatu sasa na mguu wangu umepona” anasema.
KAULI YA KITAALAMU
Dk. Moiz Vejlan ambaye ni bingwa wa mifupa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, anasema kuwa dawa za asili za mitishamba si mbaya kwa afya ya binadamu katika matumizi ya tiba, bali inategemea mgonjwa mwenyewe anavyo iamini hiyo dawa kama tiba yake.
“ Katika tiba, kila mtu ana imani yake, kuna wanao amini kuwa dawa za mitishamba ni bora kuliko za kitaalamu na wengine huamini kuwa dawa za mitishamba haziwasaidii kwa tiba” anasema Dk. Vejlani.
Mtaalamu huyoi anaeleza kuwa wataalamu wa mitishamba wamekuwa wakipata umaarufu mkubwa kutokana dawa wanazo zitumia kudaiwa kuwaponyesha wagonjwa wengi, lakini kitaalamu siyo vizuri kwani wao hutibu mgonjwa bila kujua ukubwa wa jeraha kwa undani.
“ Kwa kawaida mtu aliyevunjika mfupa lazima apigwe x-ray ili kujua ukweli na ukubwa wa tatizo, lakini kwa wenzetu wa miti shamba hilo halipo. Wao hutumia utaalamu na uzoefu walio jaliwa na Mungu wao” anasema.
Dk. Vejilani anasema Hospitali nyingi hasa za serikali zinakabiliwa na changamoto ya vifaa vya kutibu na kuunganisha mifupa, kitu ambacho kimekuwa kikiwafanya wagonjwa wengi kukimbilia kwa wataalamu wa mitishamba wakiamini kuwa hospitalini hakuna tiba.
“ Tunakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa, kitu kinacho wafanya wagonjwa wengi washindwe kuamini kuwa dawa za kitaalamu zinatibu na kukimbilia kukimbilia mitishamba” anasema.
Anashauri serikali iwatambue na kuwathamini kwa kuwaandalia mazingira mazuri wataalamu hao wa tiba a sili kwani wanawasaidia watu wengi, hususani walio vunjika viungo.
Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba ( NIMR ), Dk. Julius Massaga anasema NIR haijawahi kupokea mganga yeyote wa tiba asilia ambaye anataka kuthibitisha kuwa dawa yake ya asili inaweza kutibu mifupa.
“ NIMR kwa sasa inafanya kazi za utafiti wa dawa nyingie tu za asili lakini si zinazohusu tiba ya mifupa. NIMR haifanyi wala hakuna mganga yeyote aliyeleta maombi ya dawa yake kufanyiwa utafiti “ anasema Dk. Massaga.
TIBA YA KIMASAI
Wamasai hawako nyuma, wao ni mabingwa wa tiba asili ya mifupa; kazi ambayo wameifanya muda mrefu.
Wamekuwa wakitumia dawa aina ya ‘ beneuni’ kutibu majeraha katika mwili wa mwanadamu au mnyama.
Jina la dawa hiyo limetokana na mti wa mbeneuni ambao unaaminika kuwa na nguvu ya kuunga jeraha kwa muda mfupi na kuiacha sehemu hiyo ikikauka ndani ya saa 24.
Mtaalamu wa dawa za kimasai, Simon Ole Kipayi anasema mti wa dawa hiyo unapatikana katika sehemu chache nchini na kwamba kijiko kimoja cha chai huuzw kati ya sh. 5,000 hadi 8,000 kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutibu.
Ole Kipayi anasema kuwa mgonjwa aliyejeruhiwa au kuvunjika mfupa anatakiwa kuweka unga wa dawa hiyo kwenye jeraha na kuliacha wazi bila kufunga, kwa kuwa kama litafungwa linaweza kuoza.
“ Beneuni huivuta ngozi na kuliunganisha jeraha. Kama jeraha likikaa kwa siku tatu, utatakiwa kuosha kwanza kwenye sehemu uliyo umia halafu uweke dawa” anasema Ole Kipayi.
WENGINEO
Vero Masinga , anayeuza dawa za asili katika stendi ya mabasi ya daladala ya Mbagala Rangi-Tatu jijini Dar Es salaam, anasema mwanaye alijeruhiwa kwa panga mkononi, lakini baada ya kuitumia dawa hiyo aliyopewa na jirani yake, jeraha lilipona kabisa baada ya siku tatu.
Anasema ingawa hafahamu kama dwa hiyo imethibitishwa na wataalamu wa afya, anasema inaonyesha uwezo mkubwa wa kutibu haraka tofauti na baadhi ya dawa zitolewazo hospitalini.
“ Siku hizi ukienda hospitali kununua dwa unaweza kuuziwa dawa feki, lakini beneuni ni mti ambao mtu yeyote anaweza kuutafuta na kuuweka nyumbani kwake” anasema.
Hata hivyo, Masinga anatoa angalizo kwa wagonjwa waio fahamu dawa hiyo kuwa haitumiki kutibu mtu aliyejeruhiwa na mnyama au nyoka mwenye sumu kwa kuwa haina uwezo wa kuondoa sumu.
Alipotakiwa kuzungumzia ubora na matumizi ya dawa hizo na nyingine nchini, ofisa uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa ( TFDA), Gaudensia Simwanza anasema ofisi hiyo haihusiki na dawa za asili ila kuna idara maalumu Wizara ya Afya inayo shughulikia dawa za asili.
CHANZO : GAZETI LA MWANANCHI, TOLEO Na. 4983, Ijumaa, 14 Machi 2014.
Comments
Post a Comment