Waswahili
husema, ‘nyumba ni choo’, wakiwa na maana kuwa nyumba haiwezi kuwa kamili bila
kuwa na huduma hiyo ya choo.
Hata
hivyo, pamoja na umuhimu wa choo, lakini si kila nyumba iliyo na choo au hata
zile ambazo zina huduma hiyo, basi vyoo ni vibovu, havina hadhi. Zipo aina
mbalimbali za vyoo kwa matumizi ya binadamu katika maisha yake ya kawaida.
Vyoo
vina matumizi mengi ingawa bado watu wengi hasa katika nchi maskini na
zinazoendelea ikiwamo Tanzania wanatumia choo cha kuchuchumaa wakati wa
kujisaidia, lakini mijini na katika nchi zilizoendelea, wao hutumia vyoo vya
kukaa.
Nyumba
nyingi mijini na ofisi mbalimbali zinazojengwa hivi sasa, huwekewa vyoo vya
kukaa. Hata zile za zamani zinakarabatiwa na kubadilishwa kwa kuwekewa hivi
ambavyo vinaonekana vya ‘kisasa’.
Mgunduzi
wa vyoo vya aina hii, Thomas Crapper anasema kwa mtazamo wake aliona kukaa
wakati wa kujisaidia ni utambulisho wa ustaarabu na maendeleo.
Hata
hivyo, madaktari wanapingana naye wakisema kujisaidia katika vyoo vya kukaa
kuna madhara kiafya kwa kuwa mkao huo unaweza kuleta matokeo mbalimbali ndani
ya mwili.
Utafiti
uliofanywa na mtandao wa ‘naturesplatform’ umegundua kuwa matumizi ya choo cha
kukaa huweza kusababisha matatizo mbalimbali ikiwemo kansa ya utumbo mkubwa.
Mtaalamu
wetu wa afya wa gazeti la MWANANCHI, Samwel Shita anasema, madhara ya vyoo vya
kukaa ni makubwa kwani wakati mwingine yanaweza kuwa chanzo cha saratani ya
utumbo mkubwa kutokana na haja kubwa kubaki kwa muda mrefu katika utumbo huo.
Shita
anasema mtu anapojisaidia haja kubwa katika choo cha kuchuchumaa, kinasaidia
haja yote kutoka kwa sababu ya msukumo unaosababishwa na mkao huo.
“Unapokaa
unakuwa umekaa katika choo mwili unakuwa umelegea, hivyo inabidi utumie nguvu
kubwa kujikamua kutoa haja, tofauti na unapochuchumaa,” anasema Shita na
kuongeza:
“Matatizo
huanza hapo, unapojisaidia ukiwa umekaa na kulazimisha kujikamua unaweza
kusababisha vimishipa vidogo katika utumbo mpana sehemu ya haja kubwa ya ndani
na ya nje kuvimba na maumivu makali husababishwa na ugonjwa unaojulikana kama
‘hemorrhoid,” anasema.
Anasema
‘hemorrhoid’ ni ugonjwa ambao pia huitwa bawasiri. Mgonjwa hupata uvimbe katika
njia ya haja kubwa na hivyo kupata maumivu wakati wa kujisaidia na haja yake
mara nyingine huambatana na damu.
Aidha,
anasema vyoo hivi pia vinaweza kuwa chanzo cha magonjwa yanayotokana na
shambukizi katika utumbo mpana, kitaalamu ‘Inflammatory Bowel Disease’.
“Kila
binadamu anapaswa kujisaidia na kuhakikisha haja yote imetoka na kwisha kabisa,
inapobakia inaweza kusababisha maambukizi katika utumbo mpana kwa kuwa ule ni
uchafu wenye mchanganyiko wa vitu vingi,” anasema Shita.
“Haja
kubwa inapokuwa tayari imeshajitengeneza inapaswa kutoka yote, kama itabaki
kipindi kirefu inaweza pia kuleta uambukizi katika utumbo mkubwa na hata katika
kidole tumbo,” anasema Shita.
“Uchafu
huu si tu unaweza kusababisha maambukizi, lakini pia unaweza kuwa chanzo cha
saratani ya utumbo mkubwa. Wote tunajua kuwa mkusanyiko wa sumu mbalimbali
mwilini unakuweka katika hatari ya kupata saratani, hivyo tatizo hili
lisipotafutiwa ufumbuzi mapema linaweza kufikia huku,” anasema Shita.
Daktari
Berko Sikirov kutoka Misri ambaye alifanyia utafiti matumizi ya vyoo vya kukaa
anasema kuwa iwapo mtu ana tatizo la vivimbe vya ‘hemorrhoid’ linaweza
kumalizika iwapo ataacha kutumia vyoo vya kukaa.
Hata
hivyo, anasisitiza kuwa tatizo hili linaweza kwisha kama litakuwa katika hatua
za awali. Kwa wenye tatizo lililokomaa watalazimika kufuata matibabu kulingana
na ukubwa wake.
Dk
Sikirov anaongeza kuwa mbali na kupata vivimbe, pia mgonjwa anaweza kupata
tatizo la kutokupata choo kwa muda mrefu.
Anabainisha
kuwa kitendo cha haja kutoka kidogo na nyingine kubakia husababisha kuganda
katika ukuta wa utumbo na zoezi hilo huendelea mpaka kuwa tatizo sugu.
“Haja
kubwa huganda katika kuta za utumbo, hali hii huifanya haja izunguke kwa muda
mrefu na ndiyo tatizo hili huanzia hapa,” anasema na kuongeza:
“Unapojisaidia
ukiwa umekaa, ile njia ya haja kubwa huwa kama imejifunga, inabidi utumie nguvu
nyingi sasa ukiwa na tatizo hili la kukosa haja kubwa huifanya itoke kwa
uchache zaidi,” anasema Dk Sikirov.
Aidha,
anasema kupata haja kubwa mara kwa mara ni muhimu kwa kuwa usipoitoa maana yake
inazungusha sumu katika damu jambo ambalo ni hatari kwa afya.
Anaongeza
kuwa kutopata haja kubwa ni kichocheo chenye uwezo mkubwa wa kusababisha
saratani ya utumbo mkubwa na uambukizi katika kidole tumbo.
Tafsiri
ya kitabibu inasema hali ya kukosa haja kubwa ni pale mtu anaposhindwa kuipata
angalau mara tatu kwa wiki. Hata hivyo, ili ujue afya yako ni njema unapaswa
kuwa unapata haja kubwa angalau mara moja kila siku.
Daktari
Denis Burkitt aliwahi kuandika kitabu cha maelekezo ya chakula ili kuepuka
ugonjwa wa saratani. Katika kitabu hicho alieleza namna ambavyo watu wanaweza
kujikinga na saratani za aina mbalimbali.
Akizungumzia
saratani ya utumbo mpana pamoja na kuelezea vyakula na aina ya maisha, pia
aliwaasa watu kutumia choo cha kukaa ili kujiepusha na tatizo hilo.
Anaeleza
kuwa kwa Marekani pekee, watu zaidi ya 150,000 hufa kila mwaka kutokana na
ugonjwa wa saratani ya utumbo mkubwa.
Mtaalamu
wa Ngozi katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba Muhimbili (MUHAS),
Profesa Kisali Pallangyo anasema matumizi ya vyoo hivyo yanaweza kuwa chanzo
cha maambukizi ya magonjwa ya ngozi. Profesa Pallangyo anasema ni rahisi
kuambukizwa magonjwa ya ngono na ngozi kwa urahisi pale unapotumia vyoo vya
kukaa tofauti na vile vya kuchuchumaa.
Aidha,
anayataja magonjwa yanayoweza kuwambukizwa kwa kutumia vyoo vya kukaa kuwa ni
kaswende, harara, mba, kisonono, upele na mengine.
“Mtu
mwenye magonjwa ya ngozi au ya ngono, anaweza kuyaacha katika ‘sink’
anapolikalia, hivyo ni rahisi kwa mtu mwingine ‘kuyachukua’ mara atakapokaa
wakati wa kujisaidia,” anasema Prof Pallangyo.
Anasema
vyoo hivi ni hatari kwa afya hasa pale vinapotumika katika jumuiya na kuongeza
kuwa ni bora kutumia vile vya kukaa ili kujikinga na magonjwa.
Source:
MWANANCHI
Comments
Post a Comment